ALBERT OJWANG

    Uchunguzi wa maiti wa Albert Ojwang’, aliyefariki akiwa kizuizini katika Kituo cha Polisi cha Central jijini Nairobi, umebaini kuwa aliaga dunia kufuatia majeraha mengi mwilini.

    Mwanapatholojia wa serikali Bernard Midia, baada ya kukamilisha uchunguzi huo, alifichua kuwa Ojwang’ hakujigonga ukutani kama ilivyoripotiwa awali katika ripoti ya polisi.

    Mwanapatholojia huyo, ambaye aliendesha shughuli hiyo pamoja na mwakilishi wa familia ya Ojwang’ Mutuma Zambezi, alipuuzilia mbali uwezekano wa Ojwang’ kujijeruhi.

    Matokeo ya uchunguzi wa maiti yanakinzana na ripoti ya polisi ya Jumapili, ambapo Ojwang’ aliripotiwa kugonga kichwa chake kwenye ukuta wa seli katika Kituo hicho cha Central.

    Kwa upande wake Kinara wa ODM Raila Odinga amekilaani kifo cha Albert Ojwang’. Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 31, alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi baada ya kukamatwa kwa madai ya kuweka ujumbe wa kukera kwenye mtandao wa kijamii kuhusu afisa mkuu wa polisi.

    Ojwang’ alichukuliwa kutoka Homa Bay na kusafirishwa hadi Nairobi, ambapo alifariki katika seli za polisi.Odinga kupitia taaifa kwenye mtandao wake wa X alielezea wasiwasi wake kwamba kifo cha Ojwang ni miongoni mwa orodha ndefu ya vijana ambao wamepoteza maisha yao kwa njia tatanishi mikononi mwa maafisa wa polisi.

    Kiongozi huyo wa ODM alionya kuwa visa kama hivyo vinaondoa imani ya umma kwa wasimamizi wa sheria na serikali yenyewe.

    Waziri Mkuu huyo wa zamani alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na madhubuti kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, akisisitiza kwamba uwajibikaji si jambo la hiari.

    June 10, 2025

    Leave a Comment