Mamia ya waombolezaji walipata muda wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri wa Elimu nchini Marehemu Prof. George Magoha ambaye mwili wake ulifikishwa katika maeneo mbalimbali kutwa ya leo ili kutoa fursa ya kumuaga kabla yake kuzikwa siku ya Jumamosi.

Wakwe wa Profesa Magoha kutoka katika taifa la Nigeria walitoa heshima zao kwa densi ya kitamaduni ya kusisimua wakati wa msafara huo uliopita katika maeneo alikofanya kazi, yakijumuisha Chuo cha Sayansi ya Afya cha KNH ‚ofisi za KMPDU, ofisi za baraza la mtihani nchini KNEC‚ Shule ya Msingi ya St. Georges‚ Shule ya Upili ya Wasichana ya State House‚ Chuo kikuu cha Nairobi‚ na kumalizia katika shule ya upili ya Starehe Centre alikosomea.

Safari ya mwisho ya Waziri huyu inatarajiwa kuandaliwa siku ya Jumamosi nyumbani kwake Umiru Nyamninia, katika Kaunti ya Siaya.

February 8, 2023