Rais William Ruto mapema hii leo alikutana na kundi la Wabunge 30 wa chama cha Jubilee katika Ikulu ya Nairobi. Wabunge hao wamejitolea kufanya kazi na serikali hii ikiwa ni mara ya pili kwa wao kuhudhuria mkutano kama huo.

Rais Ruto aliapa kuunga mkono wabunge hao katika kutekeleza majukumu yao na kubainisha kuwa atatarajia watoe mkono wa usaidizi katika kufanikisha ajenda ya Kenya Kwanza.

Baadhi ya wanachama waliohudhuria ni Mbunge wa Eldas Aden Keynan, John Waluke (Sirisia), Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Sabina Chege ambaye ni mbunge mteule, Stanley Muthama (Lamu Magharibi) na Yusuf Hassan (Kamukunji) miongoni mwa wengine.

Haya yanajiri siku moja baada ya mkutano kati ya Ruto na wabunge kutoka chama cha ODM katika msingi huo huo, ambao umezua mvutano ndani ya chama hicho.

February 8, 2023