Ripoti mpya imefichua kuwa asilimia 7.4 ya watoto nchini Kenya wamesajiliwa katika gredi ya kwanza (1) bila kupata mafunzo ya Elimu ya Malezi ya Awali ya Mtoto (ECDE), hii ikionyesha mapungufu yanayoendelea katika upatikanaji wa elimu ya msingi kote nchini.
Kulingana na Ripoti hiyo ya Utafiti wa Hali ya Elimu nchini Kenya, iliyotolewa leo na Zizi Afrique Foundation na Usawa Agenda, hali hii inashuhudiwa zaidi katika maeneo ya mashinani.
Vilevile inaeleza kuwa asilimia 8.4 ya watoto mashinani wanajiunga na shule za msingi bila mafunzo ya awali, ikilinganishwa na asilimia 6.2 mijini.
Utafiti huo pia unabainisha kuwa miongoni mwa watoto ambao tayari wako katika Gredi ya 1 na kuendelea, asilimia 7.5 ya wavulana na asilimia 7.4 ya wasichana hawajawahi kuhudhuria ECDE.