Bishop John Oballa Owaa

Askofu wa Jimbo katoliki la Ngong John Oballa Owaa, amewarai wanafunzi katika shule za upili, kujiepusha na mienendo ya ulimwengu wa sasa, inayowaelekeza katika mambo yanayomchukiza mwenyezi Mungu, na hasa mahusiano ya jinsia moja. Katika tafakari yake kwenye hafla ya kubariki Mnara wa maombi wa Mchungaji Mwema katika shule ya upili ya Olchekut Supat Apostolic School eneo la Lemek kaunti ya Narok, Askofu Oballa alisema kuwa mahusiano ya aina hii ni kinyume kabisa na mapenzi ya mwenyezi Mungu, na kuwataka wanafunzi na wakristu wote kusimama imara kukabili shinikizo hili.

Zaidi ya hayo, Askofu alisisitiza kuwa mpango wa Mungu wakati wa uumbaji, ulikusudia uwepo wa uhusiano kati ya watu wa jinsia tofauti, ili kuendeleza kazi za uumbaji. Pia alitoa changamoto kwa mamia ya wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo, akiwataka kutojihusisha na mienendo na aina hii, na badala yake kufuata mwongozo wa kanisa katika kuishi maisha yao.

Mnara huo (Grotto) unatarajiwa kuimarisha maisha ya kiroho ya wanafunzi shuleni humo, Askofu akiwataka wanafunzi kuukimbilia ulinzi wake yeye aliye mchungaji mwema nyakati zote. Wanafunzi, walimu Pamoja na mapadre kutoka katika shule na parokia Jirani pia walihudhuria hafla hiyo.

February 9, 2023