Chama tawala cha UDA kimetangaza ubabe wake kwa mara nyingine baada ya wagombea wake kushinda katika maeneo 3 kati ya 4 yaliyoandaa uchaguzi mdogo hio jana.

Katika kaunti ya Murang’a Chege njuguna sasa ndiye mbunge mpya mteule wa eneobunge la Kandara, baada yake kuibuka mshindi katika uchaguzi mgogo wa ubunge ulioandaliwa hio jana. Njuguna ambaye alikuwa mwaniaji wa chama cha UDA, alijizolea kura 21,650 na kumpiku mpinzani wake wa karibu Titus Njau wa chama cha Ford Asili aliyejizolea kura 14,678.

Uchaguzi huo ulifuatia uteuzi wa aliyekuwa mbunge wa eneobunge Hilo Alice Wahome katika baraza la mawaziri. Njuguna atachukua mikoba ya kuliongoza eneo hilo kama mbunge baada ya kuapishwa kwake katika bunge la kitaifa.

Dekow amtetemesha Nassir

Kwenye eneobunge la Garissa mjini, chama cha UDA kilitetea wadhifa wa ubunge eneo hilo, baada ya Meja Mstaafu Mohammed Dekow kuibuka kidedea kwa kura 11,572 na kumpiku mpinzani wake wa karibu Nassir Mohammed wa chama cha UDM aliyejizolea kura 8,158.

Meja (Mst) Mohammed Dekow apokezwa cheti cha ushindi na afisa wa IEBC,

Wadhifa wa ubunge katika eneo hilo ulikua ukishikiliwa na waziri wa ulinzi Aden Duale. Hata hivyo shughuli za uchaguzi zilishuhudia idadi ndogo ya wapiga kura walioshiriki, tume ya IEBC ikitangaza kuwa ni asilimia 39 pekee ya wananchi waliojitokeza kupiga kura. Dekow ni mmoja wa wagombea 3 wa chama cha UDA waliosajili ushindi katika uchaguzi mdogo ulioandaliwa katika maeneo manne hio jana.

Elgeiyo Marakwet bado ni UDA

Mwingine aliyejizolea ushindi katika uchaguzi wa hio jana, ni aliyekuwa mbunge wa Marakwet magharibi William Kisang, ambaye sasa anamridhi waziri Kipchumba Murkomen kama seneta mpya wa kaunti ya Elgeiyo Marakwet. Kisang alijizolea jumla ya kura 41,378 na kumbwaga mpinzani wake Tim Kipchumba wa chama cha PPD aliyezoa kura 38,151. Kipchumba tayari amekubali kushindwa na kuahidi ushirikiano wake kwa bwana Kisang.

ODM yapata ushindi Shella

Kisiwani lamu, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa maswala ya Uvuvi katika kaunti ya Lamu Atwaa Salim alitangazwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Shella. Uchaguzi huo ulivutia wawaniaji wanne, waliokuwa wakimenyana ili kupata nafasi ya kuwawakilisha wananchi wa eneo hilo katika bunge la kaunti ya Lamu.

Atwaa Salim akabidhiwa cheti na afisa wa IEBC baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Shella.

 Salim aliyewania wadhifa huo kwa tiketi ya chama cha ODM sasa
ndiye mwakilishi wadi wa eneo hilo, baada ya kujizolea jumla ya kura
1,053 mbele ya Mohamed Hassan Ali wa Chama cha Amani National Congress
(ANC) aliyezoa kura 573. Saamiya Mohammed Abduljabar aliibuka wa tatu
kwa kura 45 huku Nizar Mohammed Shee akiibuka wa nne kwa kura 10.

January 6, 2023