Tume ya taifa ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika Desemba 20, 2023, licha ya kuzorota kwa usalama mashariki mwa nchi hiyo.

Tangazo la tume hiyo, CENI lililotolewa hii leo limekuja wakati waasi wakiendeleza harakati zao katika mkoa wa Kivu Kaskazini, katika ghasia ambazo zimewalazimisha makumi kwa maelfu ya raia kuyakimbia makaazi yao. Hata hivyo rais wa tume hiyo ameonya akisema, kuendelea kwa matatizo ya kiusalama katika baadhi ya maeneo, kutakuwa changamoto katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wazi na wa haki.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo chaguzi za rais, wabunge na serikali za mitaa hufanyika kwa wakati mmoja. Kulingana na katiba ya nchi hiyo rais mteule atachukua madaraka mwezi Januari 2024.

November 26, 2022