Aden Duale

Waziri Mteule wa Ulinzi Aden Duale amemwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula waraka wa kujiuzulu kama Mbunge wa eneobunge la Garissa mjini, kama mojawapo ya njia kujiandaa kuchukua wadhifa wake mpya.

Wengine waliotoa taarifa za kujiuzulu ni pamoja na seneta wa Elgeiyo Marakwet Kipchumba Murkomen ambaye aliteuliwa kutwaa wizara ya uchukuzi, pamoja mbunge wa Kandara Alice Wahome aliyependekezwa kuwa waziri wa Maji na unyunyizaji. Watatu hao ni miongoni mwa mawaziri wateule waliodhinishwa baada ya kuipokea ripoti ya kamati ya uteuzi siku ya jana.

Katika ripoti hiyo, wanachama walikataa kuidhinisha jina la Penina Malonza lakini wabunge katika vikao vya leo wameidhinisha majina hayo ambayo sasa yatawasilishwa kwa rais William Ruto kwa kuteuliwa rasmi kabla ya kuapishwa ili kuanza kuyatekeleza majukumu yao.

October 26, 2022