Familia ya mwanahabari mkongwe na gwiji wa utangazaji aliyeaga dunia Catherine Kasavuli, imetoa wito wa msaada kutoka kwa wakenya ili kulipa gharama za hospitali zilizofikia shilingi milioni nne zilizotumika wakati alipokua akipokea matibabu yake.

Mwanawe Kasavuli Bw. Martin Kasavuli katika waraka alioandika hio jana, amesema kuwa wamekuwa na wakati mgumu kama familia kwani wanatarajia kuwa gharama hiyo itaongezeka, hasa kutokana na gharama za maombolezi na mazishi ya gwiji huyo. Waraka huo ambao pia ulitumwa kwa baraza la vyombo vya habari nchini (MCK) umeeka wazi kuwa gharama hiyo inadaiwa katika hospitali za Kenyatta na ile ya Nairobi.

Kasavuli aliaga dunia usiku wa kuamkia jana akiwa na umri wa miaka 60 baada ya kuugua saratani kwa muda. Familia imewaomba wakenya kuungana nao katika kutoa mchango wao kupitia nambari ya Paybill ambayo ni 8089700 kwa akaunti ya Catherine Kasavuli.

December 31, 2022