Makamishna wa IEBC

Maombi manne yamewasilishwa katika bunge la kitaifa kuwataka makamishna wanne wa tume ya IEBC Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit kuondolewa ofisini.

Akiwasilisha taarifa za maombi haya, spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetangula, amesema kuwa maombi haya yaliwasilishwa na wakenya Pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, wote wakitaja sababu zao za kuwataka makamishena hawa kuondolewa katika tume ya uchaguzi nchini IEBC.

Baadhi ya sababu zilizotajwa katika maombi hayo ni Pamoja na kuwa makamishena hao walitekeleza wajibu tofauti na kiapo walichokula, kujaribu kuhitilafiana na shughuli nzima ya uhesabu wa kura za urais na kutangazwa kwa matokeo yake, Pamoja na kuandikisha hatikiapo kuunga mkono mrengo mmoja uliokua katika kinyang’anyiro cha urais.

Spika Wetangula ameiagiza Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria kuangazia maombi hayo na kutoa mwongozo kwa bunge iwapo maombi yenyewe yameafiki viwango vya kuwaondoa ofisini kamishna mmoja au wote wanne kutoka katika tume hiyo ya IEBC.

November 15, 2022