Biden COP27

Rais wa Marekani Joe Biden hii leo amewasili kwenye mji wa mwambao wa Sharm el-Sheikh nchini Misri kuhudhuria mkutano wa kilele wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP27 unaotafuta makubaliano ya kudhibiti taathira za kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani.

Wajumbe wa mkutano huo wanataraji uwepo wa rais Biden utaongeza nguvu katika kusukuma malengo ya dunia kwenye kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi licha ya matatizo yanayoukabili ulimwengu ikiwemo vita na uchumi unaochechemea. Biden anatarajiwa kutumia hotuba yake mjini Sharm el-Sheikh kuyakumbusha mataifa duniani umuhimu wa kuendelea na mipango ya kupunguza utoaji wa gesi ya ukaa na kudhibiti kupanda kiwango cha joto kupindukia nyuzi 1.5 katika kipimo cha Celsius.

Wakati wa ziara hiyo ambayo ni kituo cha kwanza cha safari ya wiki nzima kimataifa, rais Biden anatazamiwa vilevile kutangaza mipango ya pamoja na Umoja wa Ulaya kudhibiti utoaji wa gesi chafuzi ya Metani au Methane.

© https://www.dw.com/sw/idhaa-ya-kiswahili/

November 11, 2022