Viongozi wa kanisa katoliki kutoka majimbo tofauti nchini, walikongamana katika jimbo katoliki la Kakamega mchana wa leo, ili kuhudhuria hafla ya kitaifa ya uzinduzi wa kipindi cha Kwaresima mwaka wa 2023.

Kampeni ya mwaka huu kwa mujibu idara ya haki na amani inayoongoza shughuli nyingi katika kipindi hiki, itaandaliwa chini ya kauli mbiu ya Upatanisho kwa taifa shirikishi.

Askofu wa jimbo katoliki la Ngong John Oballa Owaa ambaye ni mwenyekiti wa idara ya haki na amani katika baraza la maaskofu wa kikatoliki nchini KCCB, alisema kuwa kipindi hiki kimetengwa ili kuwasaidia waumini kukoleza imani yao kwa kujikita katika mafunzo maalum yanayotolewa wakati wa kwaresima.

Kipindi cha kwaresima kinatarajiwa kuanza rasmi juma lijalo baada ya jumatano ya majivu na kuendelea kwa kipindi cha wiki tano zijazo.

 

February 17, 2023