Idara ya haki na amani katika kanisa katoliki hii leo imezindua kampeni ya kitaifa ya kipindi cha kwaresma katika shrine ya Immaculate Conception katika jimbo katoliki la Lodwar.
Kampeni hii huendana sambamba na kipindi cha kwaresima katika kanisa katoliki ambacho huanza siku ya Jumatano ya Majivu na kuendelea hadi kipindi cha pasaka.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni tujenge Kenya ya Haki, Amani na Umoja inayodumisha usawa na heshima kwa binadamu.
Mwenyekiti wa baraza la maaskofu wa kikatoliki askofu mkuu Maurice Muhatia, amewarai wakristu kujikita katika kauli mbiu ya mwaka huu na kuchagua haki na amani wakati wote.
Vilevile askofu mkuu Muhatia amewatolea wito viongozi wa kisiasa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi badala ya kuendesha kampeni za mapema, akisema kuwa kampeni hizo zinahatarisha umoja wa kitaifa.
Kuhusu suala la utawala, maaskofu wameitaka serikali kuwa na uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kutoa huduma bora za kimsingi kwa wakenya wote.

