KCCB

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini KCCB, linaitaka serikali kuzingatia kwa kina suala la mabadiliko katika sekta ya afya, ili kuhakikisha kuwa wakenya wananufaika na mabadiliko yanayofanyika. Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na KCCB katika Kituo Cha Uchungaji Cha St Mary mjini Nakuru, maaskofu wameelezea wasiwasi kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya afya.

Maaskofu wanairai serikali kuangazia kwa kina mabadiliko yanayopendekezwa katika bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), na kuhakikisha kuwa mabadiliko hayo hayawaathiri Wakenya au kuwa mzigo kwao. Aidha KCCB imeelezea kusikitishwa kwao na kucheleweshwa kwa malipo kwa vituo vya afya vinavyotoa huduma chini ya ufadhili wa NHIF.


Kuhusu suala la mabadiliko ya anga, Maaskofu wameipongeza serikali kwa kutenga siku ya kitaifa ya upanzi wa miti. Viongozi hao wamewahimiza waumini  kujitolea kushiriki katika zoezi la upanzi wa miti na kuhifadhi mazingira. Serikali ilitangaza siku ya Jumatatu 13 Novemba, kama likizo ya kitaifa ili kuwaruhusu wakenya kujishughulisha katika upanzi wa miti.

SOMA PIA: KCCB Yapendekeza Kufanyika Kwa Mabadiliko ya Katiba.

Masuala mengine yaliyojadiliwa katika taarifa hiyo ni pamoja na ongezeko la gharama ya maisha, utozaji wa ushuru wa kiwango cha juu, ukosefu wa nafasi za kazi, mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea na changamoto zinazohusu usalama, na mfumo wa elimu nchini.

Share the love
November 10, 2023