Maaskofu wa KCCB wawasilisha mapendekezo.

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini KCCB, limeeleza kwamba kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ya katiba nchini. Haya yaliwekwa wazi katika mapendekezo mbele ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa katika ukumbi wa Bomas siku ya Jumanne. Maaskofu katika ujumbe wao wameeleza kuwa mchakato huo hauwezi kufanyika haraka na unahitaji maandalizi ya kina.

Katika kikao hicho kinachoongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungw’a na Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Baraza hilo limeonyesha wasiwasi wake kuhusu vipengee vya katiba, hasa kipengee cha 43 na kipengee 26.4, ambavyo wanaviona kuwa vinaweza kuhalalisha uavyaji wa mimba. Pia, KCCB imekemea kiwango cha chini cha huduma za afya katika hospitali za umma na ufisadi katika sekta hiyo.

Maaskofu aidha wameeleza wasiwasi kuhusu mipango ya maendeleo ya serikali hasa sheria mpya ya fedha iliyoidhinishwa mwezi Julai. KCCB imependekeza kuondolewa kwa ushuru wa ujenzi wa Nyumba za bei nafuu, ikisema kwamba mpango huu huenda ukakosa kuzaa matunda yanayohitajika, hasa kwa kuzingatia jinsi mipango ya aina hii imetekelezwa katika miaka ya awali.

Kuhusu masuala ya kisiasa, viongozi hao wa kanisa katoliki wamekubaliana na wazo la kuundwa kwa ofisi ya kiongozi mkuu wa upinzani, lakini wamepinga vikali wadhifa wa mkuu wa mawaziri nchini, ambao kwa sasa unashikiliwa na Musalia Mudavadi. Pia, wamependekeza kuboreshwa kwa Sheria ya Vyama vya Kisiasa ili kuwazuia viongozi waliochaguliwa dhidi ya kuhama vyama vyao.

Ujumbe wa maaskofu uliongozwa na Padre Charles Kilonzo, Bwana John Biruri, Bi. Wanjala Nasimiyu na Bi. Costance Ntende.

Tazama Mapendekezo yote ya KCCB

 

Share the love
October 3, 2023