KCCB Mapadre Fr. Allois Cheruiyot Bett

    Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (KCCB) limelaani vikali mauaji ya mapadre wawili yaliyotokea ndani ya kipindi cha juma moja, likiitaka serikali kuhakikisha haki inatendeka.

    Kupitia Idara ya Haki na Amani (CJPD), KCCB imeeleza masikitiko yake kutokana na mauaji ya Padre John Maina Ndegwa na Padre Allois Cheruiyot Bett, na kuyataja kama vitendo vya ukatili visivyokubalika katika jamii yoyote inayojali utu wa binadamu.

    Katika taarifa hiyo iliyotolewa Alhamisi usiku, baraza hilo limehimiza vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha kwamba usalama unapatikana kwa wananchi na kutokomeza mauaji ya kiholela.

    Taarifa ya polisi iliyotolewa siku hiyo hiyo imeeleza kuwa watu sita wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Padre Cheruiyot Bett, ambaye alikuwa akihudumu katika Parokia ya Mtakatifu Matthias Mulumba Tot. Padre huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika kijiji cha Kabartile, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

    Polisi wamesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na juhudi zaidi zinafanywa ili kuwakamata washukiwa wengine. Aidha, wamelipinga dai kuwa mauaji hayo yanahusiana na visa vya wizi wa mifugo vilivyoshuhudiwa katika maeneo ya kaunti hiyo.

    May 23, 2025

    Leave a Comment