Ole Kenta Ole Ntutu Case

Vikao vya mahakama kuu ya Narok kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi wa gavana Patric Ntutu vimehairishwa kwa siku saba zaidi ili kutoa muda kwa pande zote husika kupata stakabadhi zinazohitajika katika kesi hiyo.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta, akieleza kuwa gavana wa sasa wa Narok Patrick Ntutu alihusika pakubwa na kuhitilafiana na zoezi la uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Jaji wa mahakama kuu ya Narok Teresiah Matheka alitoa muda kwa pande husika kuafikiana hasa baada ya upande wa mlalamishi unaoongozwa na wakili Pro.Tom Ojienda kuitaka tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka kutoa stakabadhi zilizohusika katika uchaguzi huo Pamoja na masanduku ya kupigia kura kwa muda wa siku nne.

Kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa Novemba 14, vita vya ubabe mahakamani vitakua kati ya Prof Tom Ojienda anayeongoza upande wa Bwana Kenta na wakili Prof Kioko Kilukumi, anayewakilisha Gavana Ntutu. Tume ya IEBC inawakilishwa na mawakili Erick Mutua na Allan Meing’ati.

Kenta hata hivyo ameeleza kuridhika na jinsi shughuli nzima inaendelea akieleza tumaini la kupatikana kwa haki. Kesi hiyo itasikilizwa tena tarehe 14 mwezi huu.

November 7, 2022