Kindiki-polisi

Maafisa wa polisi waliohudumu katika kituo kimoja cha Polisi kwa muda wa miaka 3 au zaidi watahamishwa mara moja. Haya ni kwa mujibu wa waziri wa Usalama Kithure Kindiki, ambaye amesema hatua hii inafuata kuanza kutekelezwa kwa mwongozo mpya unaoongoza utendakazi wa idara ya polisi.

Akizungumza wakati wa kikao cha kujibu maswali ya maseneta katika bunge la seneti asubuhi ya leo, Waziri huyo alitoa maelekezo kwa viongozi wa idara mbalimbali kuhakikisha kwamba uhamisho huu unatekelezwa ndani ya kipindi cha siku 60 zijazo. Waziri Kindiki aidha ameeleza kuwa wale ambao hawatatii agizo hili hawatapokea mishahara yao.

Kuhusiana na suala la utendakazi wa maafisa wa Akiba (NPR) Waziri Kindiki, amewaeleza maseneta kwamba wizara yake imeweka mikakati ya kuangazia jinsi maafisa hawa wanavyotumia silaha walizopokea kutoka kwa serikali. Hatua hii inafuata matukio kadhaa ya matumizi mabaya ya silaha hizo na maafisa wa NPR.

Kindiki alishutumu vikali visa vitatu ambapo maafisa wa NPR walitumia silaha za serikali katika vitendo vya uhalifu. Aidha, aliahidi kuwa wote watakaopatikana na hatia watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Share the love
October 11, 2023