Maandalizi ya Mashujaa

Matayarisho ya maadhimisho ya sherehe za kitaifa za Mashujaa katika Kaunti ya Kericho yamekamilika, tayari kwa hafla kubwa itakayofanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 20. Oktoba 2023.

Kilele cha maandalizi haya kilishuhudia mwanakandarasi aliyepewa jukumu la ukarabati wa Uwanja wa Kericho Green akirejesha usukani kwa serikali ya Kaunti ya Kericho baada ya kukamilisha shughuli zake za ukarabati. Hafla ya kupokea uwanja huo iliongozwa na Gavana wa Kericho, Dkt. Erick Mutai, pamoja na Waziri wa Michezo nchini Ababu Namwamba. Viongozi hawa walitoa pongezi kwa jinsi shughuli hiyo ilivyokamilika kwa muda wa miezi miwili pekee, ikionyesha dhamira ya kuendeleza miundombinu ya michezo nchini.

Sherehe za mwaka huu za mashujaa ambazo ni za 60 humu nchini, zinatarajiwa kuwa tofauti na zinajikita katika suala la afya. Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua rasmi mpango wa Afya Kwa Wote (UHC) katika sherehe hizo. Mapema siku ya Alhamisi, Rais alisaini kuwa sheria miswada minne inayohusiana na upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.

Miswada iliyofanywa sheria inajumuisha mswada wa afya ya msingi, mswada wa Huduma za Afya za kidijitali, mswada wa bima ya afya ya kijamii na mswada wa uimarishaji wa vituo vya afya.

 

Share the love
October 19, 2023