Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) imethibitisha kujiuzulu kwa Mkurugenzi Mkuu aliyesimamishwa kwa muda Ezra Chiloba .

Bodi hiyo ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Chiloba alijiuzulu siku ya Jumatano, Oktoba 18 katika barua kwa mwenyekiti wa bodi hiyo, Mary Mungai.

Kujiuzulu kwake kuliashiria mwisho wa muda wake wa miaka miwili katika mamlaka hiyo ya mwasiliano ambao ulianza Oktoba 2021. Chiloba hakuwa amefanya kazi katika Shirika hilo tangu Septemba 18, 2023, wakati ukaguzi wa ndani ulidaiwa kufichua hasara kubwa katika mpango wa CA wakati wa uongozi wake.

Kutokana na hali hiyo, alisimamishwa kazi kwa muda usiojulikana. Hata hivyo Katika barua yake Chiloba alikanusha madai hayo kuwa hayana msingi na si sahihi huku akisisitiza kwamba hatua zote zilizochukuliwa kuhusiana na usimamizi wa mpango huo wa mikopo ya nyumba zilizingatia kikamilifu sera na miongozo husika. Vilevile aliibua wasiwasi kuhusu jinsi ukaguzi wa mpango huo ulivyofanywa, akidai zaidi kuwa mchakato huo uliingiliwa.

Share the love
October 19, 2023