Maandamano ya Gen Z katika kaunti ya Narok yalichukua mkondo tofauti adhuhuri ya leo baada ya waandamanaji na maafisa wa polisi kuanza kukabiliana.
Maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria walilazimika kutumia vitoa machozi ili kuwatanya waandamanaji hao ambao walikuwa wakirusha mawe.
Watu watatu wanaripotiwa kupata majeraha ya risasi na wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Narok.
Kwingineko katika kaunti za Nakuru na Machakos, watu wawili wameuwawa kwa kupigwa risasi huku wengine wakijeruhiwa.
Maandamano sawia yameshuhudiwa pia katika kaunti za Nyeri na Kirinyaga ambapo wakaazi walijitokeza kupinga kile wametaja kama ukandamizaji kutoka kwa serikali.