Malala UDA

Katibu wa Kitaifa wa Chama tawala cha UDA, Cleophas Malala, amekanusha uvumi wa kuwepo nyufa ndani ya chama hicho. Akizungumza wakati wa ziara yake ya ufunguzi wa ofisi za chama mjini Narok siku ya Ijumaa, Malala amesisitIza kuwa hakuna chochote kinachowababaisha katika chama hicho, na pia kusifu ukuaji wa chama kote nchini.

Zaidi ya hayo, Katibu Mkuu huyo, alifichua kuwa chama hicho tayari kimewasajili wanachama zaidi ya elfu 34 katika kaunti ya Narok, na kwamba wanachama wengi wanatarajiwa kujiunga na chama hicho nchini kote. Aidha, hakuchelea kumsuta aliyekuwa Katibu wa Chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni, kwa kile alichokiita “mpango wa kuvuruga mazungumzo” kati ya serikali na Azimio la Umoja.

Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ntutu, aliunga mkono kauli hizi akisema kuwa Chama cha UDA kinaendeleza demokrasia na kutoa nafasi kwa kila mtu kuwania kiti kupitia chama hicho. Ntutu pia alithibitisha kuwa ofisi hiyo itaendelea kuwasajili wafuasi katika maeneo ya mashinani ndani ya kaunti ya Narok.

 

Share the love
September 22, 2023