Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ntutu, ameahidi kuwa serikali ya kaunti itashughulikia matatizo ya wananchi waliofurushwa kutoka msitu wa Mau mwaka 2018.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika Sogoo, Ntutu alisema serikali imeweka mipango ya kuwafidia walioathirika na kushirikiana na serikali kuu kusuluhisha changamoto za ardhi, hasa katika eneo la Chelegut ndani ya Amalo.
Alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa waliopoteza makazi wanapata fidia stahiki na ardhi mbadala, huku akisisitiza kuwa mchakato huo utafanyika kwa uwazi na haki.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Narok Kipkech Lotiatia, amewataka wakazi wa Transmara Magharibi, Mashariki na Kusini wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria kuzisalimisha mara moja.
Lotiatia alisema serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wanaotumia silaha hizo kufanya uhalifu, ikiwemo wizi wa mifugo. Aliongeza kuwa oparesheni maalum inaendelea katika maeneo hayo ili kuwakamatwa wahalifu na kurejesha hali ya usalama.
Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha usalama unaimarika na amani inadumu katika maeneo yote ya kaunti ya Narok.