Afisa Mkuu wa Afya ya Umma katika Kaunti ya Narok, Edward Tankoi, ametoa wito kwa wakazi wa wadi ya Maji Moto-Naroosura kuzingatia umuhimu wa uchimbaji na matumizi ya vyoo ili kuimarisha usafi na afya katika jamii.
Kwa mujibu wa afisa huyo, eneo hilo ni miongoni mwa yanayosalia nyuma katika utekelezaji wa matumizi ya vyoo, hali inayozuia maendeleo ya kiafya katika kaunti nzima. Ameeleza kuwa ni muhimu kwa jamii kubadilika na kuzingatia matumizi ya vyoo ili kuzuia maambukizi ya magonjwa yanayotokana na uchafu.
Kaunti ya Narok imekuwa ikikumbwa na hasara kubwa ya kifedha kutokana na gharama za kutibu magonjwa yanayoweza kuzuiwa kupitia hatua rahisi kama kuwa na vyoo safi katika kila boma.
Serikali ya kaunti kwa ushirikiano na wadau wa afya imekuwa ikitekeleza kampeni ya kuhakikisha kila wadi inakuwa na matumizi ya choo kwa asilimia mia moja, kama mojawapo ya mikakati ya kuimarisha afya ya jamii na kupunguza maambukizi ya magonjwa kama kipindupindu.
Idara ya afya katika kaunti ya Narok imeeleza kuwa ipo tayari kushirikiana kwa karibu na wananchi kwa kutoa elimu na msaada unaohitajika ili kufanikisha lengo hilo muhimu.