Peter-Salasya

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya, ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi 20,000 baada ya kuhojiwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) asubuhi ya leo. Kuachiliwa huko kunafuatia madai ya kumtishia maisha Hakimu Gladys Kiama wa Mahakama ya Kakamega.

Bw. Salasya, aliyewasili kwenye ofisi za DCI mjini Kakamega na kuhojiwa kwa muda wa saa mbili, amekanusha vikali madai hayo. Amesema kuwa anakabiliwa na tuhuma za kisiasa na kwamba shutuma hizo ni njama ya kumharibia jina lake.

Salasya aliombwa kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi baada ya Hakimu Kiama kuwasilisha taarifa akidai kutishiwa maisha baada ya uamuzi wa kesi inayohusisha mbunge huyo ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza. Akizungumza na wanahabari baada ya kuhojiwa, Salasya amesema kwamba kuna njama ya baadhi ya watu kukabiliana naye kisiasa, na kumharibia jina, akisema hakumtishia kwa vyovyote hakimu Kiama.

December 5, 2023