BY ISAYA BURUGU 4TH DEC 2023-Mshtuko umetanda katika kijiji cha Kianjege huko Ndia, Kaunti ya Kirinyaga leo  baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 47 ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi kumuua rafiki yake mwalimu mstaafu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 65 na kujisalimisha mwenyewe kwa polisi.

Kulingana na jamaa za mshukiwa, Elijah Wanjohi alimpigia simu dadake mkubwa asubuhi na kumwambia ampeleke katika kituo cha polisi cha Kianjege kwa sababu alikuwa amemuua rafiki yake na mwili wake ulikuwa umelazwa katika boma lake.

Wakazi walioshtuka wamesema hawakuamini kwamba Wanjohi angeweza kumuua rafiki yake, Caxton Mbuthia, kwa vile wawili hao walikuwa marafiki wakubwa.

Njeri amewambia wandishi habari kwamba miezi mitatu iliyopita, alimpeleka kakake katika kituo cha kurekebisha tabia kwa sababu ya unywaji pombe kupita kiasi.

Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Ndia  Moses Koskei amesema mwalimu huyo alitumia uma jembe kumuua rafiki yake.

Mkuu huyo wa polisi ameongeza kuwa  Wanjohi amepelekwa katika kituo cha polisi cha Baricho ambako anahojiwa huku mwili wa mwathiriwa ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Karatina kwa uchunguzi.

 

December 4, 2023