Ajali

Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 63, ambaye ni mhudumu wa boda boda, amefariki na mwingine kujeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani Mjini Narok. Ajali hiyo ilitokea karibu na Mahakama ya Narok kwenye Barabara Kuu ya Narok – Mau, baada ya gari aina ya Toyota Rav4 kugongana uso kwa uso na pikipiki iliyokuwa na mhudumu mmoja pamoja na abiria wake.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Narok, Kizito Mutoro, alithibitisha kisa hicho na kueleza kwamba ajali hiyo ilisababishwa na jaribio la dereva wa gari la Rav4 kupita gari lililokuwa mbele yake. Ajali hiyo ilisababisha majeraha mabaya kwa wanaume hao wawili ambao walikimbizwa haraka katika Hospitali ya Rufaa ya Narok kwa matibabu.

Mhudumu wa boda boda alipokea matibabu katika hospitali hiyo, lakini kwa kusikitisha, alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata. Mwili wake umehifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika Hospitali hiyo.

 

 

 

November 3, 2023