Chama cha Wafanyakazi (COTU-K) kimetaka Mamlaka ya Afya ya Kijamii SHA ipewe uhuru kamili wa mifumo yake. Katika taarifa Jumanne, Katibu Mkuu Francis Atwoli, alisema COTU kwa muda wa mwezi mmoja uliopita imekuwa ikitafuta mkutano na Waziri wa Afya Aden Duale ili kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikikabili bima hiyo ya SHA, ila hawajafanikiwa.

    COTU inahoji kuwa kikwazo kikubwa cha SHA ni kutegemewa kwa mfumo wa TEHAMA ambao ni tofauti na mamlaka ya kuendesha shughuli zake, huku udhibiti huo ukiwa mikononi mwa Wizara ya Afya (MoH) na Mamlaka ya Afya ya Kidijitali (DHA).

    Kulingana na muungano huo, mamlaka hiyo inahitaji kuwa na udhibiti wa miundombinu yake ya kiteknolojia katika kutekeleza uhuru wake kutoka kwa wizara na DHA.

    Mwingine kutilia doa mifumo ya SHA ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ambaye anasema kuna majaribio ya kimakusudi kuficha hasara ya mamilioni yaliyotolewa kwa vituo vya afya hewa na Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).

    Akihutubia wanahabari Jumanne, Maraga alibainisha kuwa siku ya Jumatatu, tovuti ya Usajili wa Kituo Kikuu cha Afya ya Kenya (KMHFR) ilifutwa katika majaribio ya makusudi ya kuficha madai ya ulaghai katika SHA.

    Jaji Mkuu huyo wa zamani sasa anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza upotevu wa fedha kupitia malipo ya madai ya matibabu.

    Maraga alishangaa ni kwa nini tovuti hiyo ilikumbwa na hitilafu baada ya ufichuzi kuwa mamilioni ya pesa yalitolewa kwa vituo vya afya visivyokuwepo na visivyofanya kazi kote nchini.

    August 26, 2025

    Leave a Comment