BY ISAYA BURUGU 8TH DEC 2022-Maafa yamekumba familia moja katika eneo la Mumoni, Mwingi Kaskazini, kaunti ya Kitui baada ya teksi ya kukodi aina Probox iliyokodishwa kusafirisha mwili hadi kwenye mazishi kupinduka na kumuua mmoja wa waombolezaji.

Ajali hiyo ilitokea kando ya barabara ya Mwingi-Kyuso, takriban mita 300 kutoka kwa daraja la Kamuwongo dakika chache baada ya saa sita adhuhuri.

Chifu wa Kamuwongo, Jane Mwende, ambaye alikuwa miongoni mwa waliofika katika eneo la tukio mapema alisema gari hilo lilibingiria mara kadhaa na kumwaga sanduku la mwili kabla ya kupinduka kuangalia juu.

Picha:Hisani

Alisema dereva wa gari hilo alishindwa kulidhibiti baada ya tairi la mbele kupasuka. Aliongeza kuwa mwanamke mwombolezaji alikufa papo hapo.

Hatima ya waombolezaji wengine ambao walikuwa kwenye gari hilo na dereva haikufahamika mara moja kwani inasemekana walikimbia kwa mshtuko.

Hata hivyo, chifu alisema alifahamishwa kuwa waombolezaji hao walikuwa wakielekea kwenye mazishi katika kijiji cha Katooni, eneo la Mumoni msiba ulipotokea.

December 8, 2022