Katika kijiji cha Ololulunga, Narok Kusini, simulizi ya Nampayo Koriata ni ushuhuda wa maumivu yaliyogeuzwa kuwa matumaini. Nampayo ni mwanzilishi wa Nampayo Koriata Fistula Trust, shirika linalobadilisha maisha ya wanawake wanaoishi na ugonjwa wa nasuri (fistula) na waathiriwa wa ukeketaji.
“Mimi ni msichana niliyekua na afya nzuri hadi mwaka wa 1999 ndipo maisha yalianza kuleta changamoto. Nakumbuka tarehe 22 Novemba mwaka huo nilikeketwa na kisha nikarejea shuleni nikiwa katika darasa la sita,” anasema Nampayo.
Baadaye, akiwa shuleni, alijaribu kuiga maisha ya wasichana wenzake kwa kile anasema ni kujihusisha na wavulana. Hatua hiyo ilisababisha apate ujauzito akiwa na umri mdogo. “Nilipojifungua sikujua kama nimepata nasuri. Mwanamke wa Kimaasai au msichana anapojifungua hupewa mafuta. Mimi nilipopewa mafuta nilishindwa kuzuia kwenda haja, nilishtuka tu,” anakumbuka.
Hali hiyo ilimfanya akataliwe na jamii. Badala ya kukata tamaa, alianzisha Nampayo Koriata Fistula Trust kusaidia wanawake wengine walioathirika. Shirika lake linatoa mafunzo kuhusu ugonjwa wa nasuri, huduma za afya na stadi za kiuchumi kama ufugaji nyuki, kilimo cha mboga na ushonaji wa shanga. Pia anatetea vikali kukomeshwa kwa ukeketaji wa wasichana.
Elizabeth Sankei na Joana Mututuae, wanachama wa kikundi cha Nalang’u, wanasema wamepata manufaa makubwa. “Mradi wake wa Fistula umetusaidia sana. Wengi wetu tulipitia changamoto kama hizi na hatukujua namna ya kukabiliana nazo. Sasa tumepata ujuzi,” asema Sankei.
Joana anaongeza: “Kina mama wamekuwa wakipata pesa za kujiendeleza kupitia miradi ya kupanda mboga na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.”
Kwa Nampayo, makovu ya maisha yamekuwa chanzo cha nguvu. Kupitia Nampayo Koriata Fistula Trust, anapanua huduma zake ili kuhakikisha wanawake zaidi wanapata tiba, msaada na matumaini, huku akipigania jamii isiyo na unyanyapaa na ukeketaji.