Wakenya wanaotarajia kupata afueni kutokana na bei ya bidhaa za petroli wamepata pigo baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la kupinga serikali kushughulikia bei ya mafuta.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa Desemba 2023 na Kituo cha Sheria ilishtumu Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) na Wizara ya Nishati kwa kushindwa kupunguza gharama ya mafuta licha ya kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Ombi hilo lilisema kuwa kushindwa kuchukua hatua kumesababisha gharama ya maisha kuwa juu zaidi hali ambayo imepunguza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Katika uamuzi wake hata hivyo, jaji Chacha Mwita aliamua kwamba walalamishi hawakuthibitisha jinsi EPRA na Wizara ya nishati zilivyokiuka haki za kiuchumi na za wateja kama ilivyoainishwa chini ya Ibara ya 43 na 46 ya Katiba.
Uamuzi huu unamaanisha kuwa bei ya mafuta itaendelea kuamuliwa chini ya mfumo uliopo wa bei.