Papa Francis

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, ameeleza kwamba hana nia ya kujiuzulu kutoka kwa wadhifa huo, akisema kwamba afya yake inamruhusu kuendelea na majukumu yake. Kauli hii imetolewa kupitia kitabu kipya ambacho dondoo zake zimechapishwa katika gazeti la Italia, Corriere della Sera.

Papa Francis ameitaja fikra ya kujiuzulu kuwa ni ndoto, akisisitiza kwamba hana sababu yoyote ya kumpelekea kufanya hivyo. Papa huyo mwenye umri wa miaka 87, amekuwa akiendelea na majukumu yake licha ya changamoto za kiafya.

Ingawa amekuwa akiugua na hivyo kupelekea kutumia vifaa vya msaada kama vile kiti cha magurudumu au mkongojo, Baba Mtakatifu Francis ameendelea kuwa imara katika kutekeleza majukumu yake ya kidini. Aidha, amekuwa akipunguza shughuli zake za umma kutokana na hali yake ya kiafya, lakini bado anaendelea kujitolea kwa umma kwa kadri inavyowezekana.

March 14, 2024