Papa Leo XIV amekubali kujiuzulu kwa Askofu Paul Kariuki Njiru, Askofu mwanzilishi wa jimbo Katoliki la Wote. Katika uamuzi huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Msaidizi wa sasa wa Wote, askofu Simon Peter Kamomoe kama Msimamizi wa Kitume, akimkabidhi jukumu la uchungaji na utawala wa jimbo hilo katika kipindi hiki cha mpito.
Tangazo hilo lilitolewa Roma, tarehe 25 Machi 2026, saa 12:00 adhuhuri (saa za Vatikani),na liliwasilishwa rasmi kwa Maaskofu wa Kenya kupitia mwakilishi wa papa nchini Kenya, Askofu Mkuu Bert Van Megen.Katika siku za hivi karibuni, Askofu Kariuki amekabiliwa na changamoto za kiafya, jambo ambalo limechangia usaidizi kutoka kwa askofu msaidizi.
Kujiuzulu kwa Askofu Kariuki kunaashiria mwisho wa sura muhimu katika historia ya Wote, Jimbo alilosaidia kuihuisha. Aliteuliwa tarehe 22 Julai 2023 na Papa Francis, akawa askofu wa kwanza wa jimbo hilo. Alisimikwa tarehe 30 Septemba 2023, akiashiria mwanzo wa safari mpya ya kikanisa katika Kaunti ya Makueni.
Alizaliwa tarehe 11 Machi 1963 huko Kathunguri, Kaunti ya Embu, wito wa Askofu Kariuki umeundwa kupitia njia thabiti ya malezi na huduma. Alisoma Falsafa katika Seminari ya Mtakatifu Yosefu, Meru, na Theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Thomas Aquinas, Nairobi, kabla ya kutawazwa kuwa Padri tarehe 1 Machi 1993.
Kabla ya kuteuliwa kwake Wote, Askofu Kariuki alihudumu kama Askofu wa Embu kuanzia 2009 hadi 2023, kufuatia kuteuliwa kwake na Papa Benedict XVI. Katika kipindi hiki, alijitofautisha kupitia uongozi wa kichungaji na maendeleo ya kitaasisi, ikiwa ni pamoja na nafasi yake kama Mwenyekiti wa Tume ya Afya ya Kikatoliki ya Kenya, ambapo alisimamia mtandao mpana wa vituo vya afya vinavyoendeshwa na Kanisa.

