Kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, amesema kuwa muungano huo hautambui uhalalai wa uongozi wa Rais William Ruto. Odinga alikua akizungumza katika uwanja wa Kamukunji baada ya kuwaongoza wananchi Pamoja na viongozi wengine wa muungano huo katika baraza la umma mchana wa leo.

Muungano huo umeshtumu jinsi tume ya IEBC iliendesha uchaguzi mkuu, na sasa wanaitaka serikali ya Kenya kwanza Kujiuzulu wakisema kwamba haiku madarakani kwa njia za halali. Odinga ametangaza kuyapinga matokeo ya uchaguzi uliopita, na kusema kuwa uongozi wa serikali ya sasa haitambuliki na wanachama wa muungano huo.

Zaidi ya hayo, Bwana Odinga ambaye alirejea nchini asubuhi ya leo kutoka katika ziara ya kikazi katika taifa la Afrika Kusinii, alieleza kuwa hana haja na kupata nafasi za uongozi katika serikali ya Kenya Kwanza, akisema kuwa ripoti ya mfichuzi iliyochapishwa imewapa uhakika kuwa aliibuka mshindi katika uchaguzi wa urais wa mwaka jana.

Kwa upande mwingine, Rais William Ruto amesema kuwa taifa la Kenya halitakubali kutekwa nyara ili kushughulika na maswala ya watu wachache humu nchini, badala yake akiweka bayana kwamba serikali yake itawatumikia wakenya wote bila ubaguzi.

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya dadake Waziri wa biashara Moses Kuria, Bi. Pauline Nyokabi Kuria eneo la Gatundu katika kaunti ya Kiambu, Ruto ameonekana kumsuta kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, akieleza kuwa vitisho vya maandamano havitazaa matunda yoyote kwa viongozi wa upinzani kupenyeza katika serikali.

Rais pia ametuma majibu yake kwa Viongozi wa muungano wa Azimio waliosema kuwa hawatatambua uongozi wake, akisema kuwa mbinu wanazotumia katika kutafuta kile alichokiita “handshake” hazitafaulu.

January 23, 2023