Kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, ametangaza kuwa ataandaa baraza la mashauriano la umme siku ya jumatatu tarehe 23 mwezi huu katika uwanja wa Kamukunji.

Taarifa kutoka kwa ofisi ya msemaji wa bwana Odinga imeeleza kwamba kikao hicho kinatarajia kuzungumza kuhusu ripoti ya mfichuzi iliyotolewa hivi majuzi ikieleza kuhusu kile kinachotajwa kama uovu uliotukia katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Tayari viongozi wa muungano huo wamekua na vikao vya waandishi wa habari kueleza kuhusu ripoti hiyo na ujio wa kinara wao unatarajiwa kueleza mkondo ambao muungano huo unatarajia kuchukua.

Odinga amekua nje ya taifa kwa shughuli za kikazi katika taifa la Afrika Kusini kama Mwakilishi Mkuu wa Muungano wa AU katika maswala ya Miundombinu barani Afrika.

January 21, 2023