Jimbo katoliki la kitale limepata askofu mpya baada ya kusimikwa kwa padre Henry Juma Odonya kama askofu wa jimbo hilo.

Askofu Odonya, aliteuliwa kwenye wadhfa huo na papa Francis mwezi Novemba mwaka jana baada ya kustaafu kwa askofu wa jimbo hilo Maurice Anthony Crowley aliyehitimu umri wa kustaafu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, mwakilishi wa papa nchini Kenya na Sudan Kusini askofu mkuu Bern Van Megen alimhimiza askofu Odonya kuwa kama daraja kati ya Mungu na Waumini anapotekeleza jukumu lake la kueneza injili.

Kabla ya uteuzi wake kama askofu, alifanya kazi kama Mwanzilishi katika Jumba la Falsafa la St. Patrick huko Durban, Afrika Kusini. Askofu Odonya Alitawazwa kama shemasi mwaka wa 2005, na mwaka mmoja baadaye akatawazwa kuwa kasisi mnamo Juni 25 katika Kanisa la Sacred Heart Cathedral Eldoret.

Amewahi kuwa padre msaidizi katika parokia ya Mtakatifu Patrick Kapcherop mwaka 2006-2007 kisha mwaka wa 2008 hadi 2009 akawa padre msaidizi wa parokia ya Mtakatifu Teresa wa Avilla Ndalat.

Mwaka wa 2009-2011, alihudumu kama Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Patrick Kapcherop katika Jimbo Katoliki la Eldoret. Kuanzia 2012 hadi 2015 askofu Odonya alikuwa mwenyekiti wa muungano wa Fidei Donum nchini Kenya na kati ya 2015 hadi 2016 akawa mwenyekiti wa Jumuiya ya Mapadre ya jimbo la Eldoret.

January 21, 2023