Kiongozi wa taifa Rais William Ruto ameahidi kuimarisha tume huru na idara zilizoundwa kikatiba, ili kuziwezesha kutekeleza wajibu wake kwa njia inayofaa, huku pia akiahidi kuwa serikali yake haitajihusisha kwa vyovyote na kuhitilafiana na tume hizo.

Akizungumza katika kikao cha mashauriano na viongozi wa tume huru na idara zingine za serikali katika ikulu ya Nairobi, Rais amesema kuwa serikali kupitia kwa wizara husika itazipa rasilimali za kutosha tume hizi ili kuzipa nguvu ya kuwatumikia wakenya ifaavyo. Rais ameongeza kuwa tume hizi zinachangia pakubwa katika mafanikio ya serikali yoyote ile.


Wakati wa hafla hiyo, mwenyekiti anayeondoka wa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC Wafula Chebukati, alimkabidhi rais William Ruto Ripoti ya shughuli ya uchaguzi mkuu uliokamili, pamoja na stakabadhi nyingine muhimu ambazo tume hiyo ilitumia katika kutekeleza wajibu wake wakati wa uongozi wa Chebukati.

Akizungumza katika kikao hicho, Chebukati ambaye kipindi chake ofisini kinakamilika leo amesisitiza kwa mara nyingine kuwa aliendesha uchaguzi mkuu uliokamilika kwa njia ya uwazi Zaidi licha a changamoto nyingi zilizokuwa zimemkodolea macho.

Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Rais William Ruto alisifia Chebukati na makamishena wenzake wawili wanaoondoka ofisini, kwa kusimama kidete na haki wakati wa uchaguzi licha ya ahadi na vitisho vingi walivyokutana navyo.

Viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini akiwemo Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, mwenzake wa Seneti Amason Kingi na mwanasheria mkuu Justin Muturi miongoni mwa wengine walihudhuria hafla hiyo.

January 17, 2023