Kamati ya kitaifa inayohusika na maandalizi ya hafla za kitaifa, inapania kujenga uwanja mpya wenye uwezo wa kusheheni wananchi 20,000 katika kaunti ya Embu, kama mojawapo ya njia za kujiandaa kwa maadhimisho ya sherehe za Madaraka mwaka huu katika kaunti hiyo.

Akizungumza baada ya ya ukaguzi wa nyuga mbalimbali katika kaunti ya Embu, Katibu mkuu katika wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo ameeleza kuwa matayarisho ya kujenga uwanja mpya katika uga wa Njukiri yameanza mara moja. Uwanja huo ambao umekuwa ukitumika kuandaa maonyesho ya kila mwaka ya kilimo, sasa utainuliwa hadhi na kuweza kuwekwa ukubwa wa kutoshea wananchi 20,00 na magari 5,000.

Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi tano ijayo, ili kuandaa sherehe hizo kwa mujibu wa agizo la rais mwaka jana katika maadhimisho ya sherehe za Jamhuri. Sherehe hizo zitajikita katika maswala ya Afya.

January 17, 2023