Jeshi la Wanahewa

Rais William Ruto leo anatarajiwa kuongoza hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Wanahewa la Kenya. Sherehe hizi zinatarajiwa kufanyika katika kambi ya Moi Airbase, Eastleigh, jijini Nairobi.

Kiongozi wa taifa, ambaye amekuwa katika ziara ya kikazi nchini Korea Kusini, alirejea nchini Ijumaa 7.06.2024, ili kuhudhuria hafla hii muhimu. Katika hafla hiyo, Jeshi la Wanahewa litapata fursa ya kuonyesha uwezo wao na kusherehekea mafanikio yao katika miongo sita tangu walipoanza kutekeleza majukumu yao ya kulinda taifa.

Jeshi la Wanahewa la Kenya lilizinduliwa rasmi tarehe 1 Juni, 1964, siku ambayo pia inaendana na maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Madaraka. Tangu wakati huo, jeshi hili limeendelea kukuza uwezo wake na kutoa mchango mkubwa katika usalama wa anga wa nchi. Jeshi hilo linatarajiwa kutoa maonyesho mbalimbali yanayolenga kuonyesha ufanisi wao katika sekta ya ulinzi wa anga.

June 8, 2024