Rais William Ruto anatarajiwa kuzuru kaunti ya Narok asubuhi ya leo ili kukagua na kuthamini miradi ya maendeleo aliyozindua hivi majuzi katika kaunti hii.
Baadaye, Rais atatembelea Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara kwa lengo la kuwaalika watalii kutoka mataifa mbalimbali wanaozuru eneo hilo, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kupanua sekta ya utalii nchini. Hatua hii inalenga kuongeza mapato ya taifa kupitia fedha za utalii huku taifa likijitahidi kukuza uchumi na kuunda nafasi za ajira kwa wananchi.
Rais ataandamana na Gavana wa Kaunti ya Narok Patrick Ntutu, Waziri wa Utalii Rebecca Miano, pamoja na Katibu katika Wizara ya Utalii John Olooltua miongoni mwa viongozi wengine serikalini.
Ziara hiyo itampeleka Rais katika Uwanja wa Ndege wa Iloisiusiu, viungani mwa mji wa Narok, eneo la Sekenani, na hatimaye katika Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara.
Ziara ya Rais inafanyika siku chache baada ya Mbuga ya Maasai Mara kutambuliwa rasmi na kuingia katika vitabu vya kumbukumbu vya World Book of Records, hatua inayoendeleza hadhi ya mbuga hiyo duniani na kuipa Kenya nafasi kubwa katika sekta ya utalii wa kimataifa.