Serikali imepiga marufuku utoaji wa leseni kwa baa tisa katika eneo la Nchurra Eobori, kaunti ndogo ya Narok ya Kati. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kina mama kuandamana wakilalamikia kuongezeka kwa uuzaji wa pombe haramu katika eneo hilo.
Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Narok ya Kati, Kennedy Mwangome, amesema marufuku hiyo inalenga kukabiliana na ukiukaji wa sheria kuhusu uuzaji wa pombe. Ameonya kuwa hatakubali utoaji wa leseni kiholela kwa maeneo ya burudani ambayo yanakiuka masharti.
Kando na hayo Mwangome amependekeza kubuniwa kwa kamati ya kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya mashinani. Amesisitiza kuwa mafanikio ya juhudi hizi yatategemea ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa na kushiriki mikakati ya kukomesha pombe haramu.
Kamanda wa Polisi wa Narok ya Kati, John Momanyi, ameunga mkono uamuzi huo. Momanyi amesema serikali itachukua hatua za haraka kuwalinda wanafunzi dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya.
Wakati wa maandamano hayo, kina mama walieleza kuwa waume zao wengi hutumia muda mwingi katika baa mchana kutwa. Walidai hali hiyo imeathiri familia zao kwa kiasi kikubwa, huku vijana wengi wakijihusisha na uraibu wa pombe.
Aidha, kina mama hao walieleza kuwa baadhi ya watoto wamelazimika kuacha shule kwa sababu ya wazazi wao kutumia pombe kupita kiasi. Wamesema hali hiyo inatishia mustakabali wa kizazi kijacho.