Wazazi walio na wanafunzi wanaoendelea na masomo yao chini ya mtaala mpya wa elimu wa CBC, sasa wamepata kupumua baada ya taarifa ya jopokazi lililotwikkwa jukumu la kukusanya maoni kuhusu mtaala huo kuwasilisha ripoti yake kwa rais William Ruto.

Ripoti hiyo ya uchunguzi huo wa muda mfupi, imeweka bayana kwamba wanafunzi wanaokamilisha mitihani yao ya gredi ya Sita wataendelea na masomo yao Gredi ya saba, japo hawatahitajika kuhama kutoka shule zao za sasa hadi katika shule zingine kwani gredi za saba na nane zitasalia katika shule za msingi.

Taarifa iliyowasilishwa kwa rais Ruto katika ikulu ya Nairobi siku ya Alhamisi, aidha imeweka bayana kwamba, mtihani wa kitaifa wa KPSEA uliokamilika hio jana hautatumika kuamua iwapo wanafunzi watapiga hatua mbele katika gredi ya saba, ila utatumika kutathmini kiwango cha ufahamu cha mwanafunzi na jinsi anaendelea masomoni, na hivyo kutoa mwongozo kwa mwalimu kuhusu jinsi mwanafunzi anahitaji kupata msaada.

Ripoti hiyo aidha imeweka wazi kuwa serikali itawaajiri waalimu 30,000 zaidi mwezi januari mwaka ujao, watakaosaidia katika kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa gredi ya saba. Ripoti kamili ya jopokazi hili inatarajiwa kutolewa mwezi machi mwaka ujao.

December 2, 2022