Tanzania x

    Tanzania inaripotiwa kuzima matumizi ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), saa chache baada ya akaunti kadhaa rasmi kudukuliwa na kusambaza taarifa za kupotosha.

    Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya NetBlocks, ambayo hufuatilia upatikanaji wa huduma za mitandao duniani, huduma ya mtandao wa X haipatikani nchini Tanzania kupitia mitandao ya simu kama Vodacom, Airtel, Halotel, pamoja na watoa huduma wengine kama Liquid Telecom na Habari Node.

    Tukio hili limefuatia mashambulizi ya kidijitali dhidi ya akaunti muhimu za serikali na taasisi za umma. Akaunti rasmi ya Jeshi la Polisi Tanzania, akaunti ya kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania, pamoja na ile ya chama tawala CCM, ziliripotiwa kudukuliwa.

    Wadukuzi walitumia akaunti hizo kusambaza jumbe zenye madai ya uongo, ikiwemo taarifa ya kutungwa kuhusu kifo cha Rais Samia Suluhu Hassan.

    Kuzimwa kwa mtandao huo kunajiri wakati hali ya kisiasa nchini Tanzania ikizidi kuwa tete. Wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu kutoka Kenya waliokuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, wameripotiwa kukamatwa au kufukuzwa nchini humo.

    Hatua hiyo imeibua maswali kuhusu uhuru wa kujieleza na nafasi ya mitandao ya kijamii katika kutoa taarifa na kufuatilia masuala ya kisiasa.

    Hadi sasa, serikali ya Tanzania haijatoa tamko lolote rasmi kuhusu kuzimwa kwa huduma ya mtandao wa X au lini huduma hiyo itarejeshwa.

    May 21, 2025

    Leave a Comment