Tume ya Huduma za Mahakama JSC imetangaza nafasi katika Afisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama huku muhula wa mhudumu wake wa sasa Anne Amadi ukikaribia kukamilika.

Katika tangazo lililochapishwa Jumatatu, Tume hiyo ilifichua kuwa muda wa Amadi unatarajiwa kuisha tarehe 13 Januari 2024.Kulingana na JSC, uteuzi huo utafanywa kwa mujibu wa kifungu cha 161(2)(c) cha Katiba.

Tume hiyo aidha imewataka watu wanaovutiwa na waliohitimu kutembelea tovuti ya JSC ili kupata maelezo ya kina kuhusu kazi hiyo, mahitaji ya kuteuliwa na maagizo ya jinsi ya kutuma ombi.

Maombi yote yanapaswa kufika kwa tume hiyo kabla ya tarehe 13 Novemba 2023, saa kumi na moja jioni. Mgombea atakayefaulu atahudumu kwa muda wa miaka mitano na muda huo unaweza kurefushwa kulingana na utendakazi.Amadi, alichukua nafasi hiyo Januari 2014 kutoka kwa Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gladys Boss.

October 23, 2023