Mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kitaifa Kimani Kuria amewasilisha bungeni ripoti ya maoni ya wakenya kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Wabunge watapata fursa ya kujadili ripoti hiyo kabla ya kupiga kura ya kuuidhinisha au kuuangusha siku ya Alhamisi. Aidha mapema leo, Kuria aliweka wazi baadhi ya marekebisho yaliyofanywa kwenye mswada huo wakizingatia maoni ya wakenya waliyokusanya wakati wa zoezi la kukusanya maoni kuhusu mswada huo.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya fedha alisema kuwa baadhi ya ushuru ambao umeondolewa kwenye mswada huo ni pamoja na ushuru wa asilimia 16 kwenye bidhaa za mkate na ushuru wa magari. 

Kando na hayo, Kuria aliongeza kuwa ushuru wa kutunza mazingira maarufu Eco-levy unaotozwa bidhaa kama vile Sodo na magurudumu, umeondolewa kwenye bidhaa zinazotengenezwa humu nchini na sasa utatozwa tu kwenye bidhaa zilizokamilika ambazo zinaingia humu nchini kutoka mataifa mengine.

June 18, 2024