29TH DEC,2023- Wakenya hawajaridhishwa na utendakazi wa jumla wa Rais William Ruto na utawala wake mwaka mmoja madarakani.Haya ni kulingana na kura ya maoni ya mwisho wa mwaka iliyofanywa na kampuni ya utafiti ya Infotrak ambayo matokeo yake yalitolewa Ijumaa.

Wakenya walioshiriki katika utafiti huo uliofanywa tarehe 18 Desemba – 19 Desemba, walikadiria utendakazi wa jumla wa Rais Ruto mnamo 2023 katika daraja la D huku naibu wake Rigathi Gachagua akipata alama za chini zaidi za daraja la E.

Umma pia ulionekana kuchukizwa na utendakazi wa Makatibu wa Baraza la Mawaziri, Bunge la Kitaifa, Seneti, Mahakama, polisi, upinzani na serikali za kaunti, huku wote wakipewa daraja D.

Kulingana na kura hiyo, suala kuu la Wakenya walio wengi kwa asilimia 56 na ambalo wanataka lishughulikiwe ni suala la kipaumbele ni gharama ya juu ya maisha.Asilimia 36 ya Wakenya wana wasiwasi kuhusu ushuru mkubwa unaofuatwa na gharama ya mafuta kwa asilimia 33, ukosefu wa ajira (27%), upatikanaji wa huduma za afya nafuu (15%), ufisadi (13%) na usalama wa chakula (13%).

Utafiti huo unaonyesha zaidi kwamba ikilinganishwa na Desemba 2022, idadi ya Wakenya wanaohisi kuwa nchi inaelekea pabaya imeongezeka kwa asilimia 7 kutoka asilimia 55 hadi asilimia 61.

 

December 29, 2023