Watu 42 wamethibitishwa kufariki baada ya mafuriko makubwa kusomba nyumba kadhaa katika Kijiji cha Kamuchiri Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Kulingana na OCPD wa Naivasha Stephen Kirui, watoto 17 ni miongoni mwa waliofariki.Kuna hofu kuwa huenda idadi hii ikaongezeka huku makumi ya watu wakiwa hawajulikani waliko kufuatia kisa hicho cha saa 10 asubuhi kilichowapata waathiriwa wakiwa wamelala.

Kisa hicho kilitokea baada ya bwawa la msimu kuvunja kingo zake na kufagia nyumba hizo.Kufuatia kisa hicho, sehemu za barabara kuu ya Mai Mahiu-Suswa/Narok na Barabara ya Mai Mahiu-Naivasha zimefungwa.

Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) na maafisa wa Kaunti wanasafisha matope na magogo ambayo maji yanayotiririka yalikuwa yamesomba.

Madereva wanaotumia njia zilizoathirika wameshauriwa kutafuta njia mbadala baada ya mvua kunyesha na kusababisha sehemu za barabara kutopitika.

April 29, 2024