26TH DEC,2023-Watu wanne wamefariki papo hapo  baada ya dereva wa lori kupoteza mwelekeo na kupelekea lori lake kuacha Barabara  na kuwagonga wanne hao katika eneo la Bulemia huko Budalangi kaunti ya Busia.Polisi wanasema Lori hilo lilikuwa likiendeshwa katika Barabara ya  Mundere Port Victoria  wakati ajali hiyo ya leo asubuhi ilipotokea. OCPD wa Bunyala Isaya Mose amesema uchunguzi unaendelea ili kuwatia mbaroni dereva wa lori husika na otingo wake.

Kwingineko  msichana wa miaka 13 alifariki papo hapo  huku mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 23 akijeruhiwa usiku wa kuamkia leo baada ya wawili hao kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi katika Kijiji cha  Ndandi , Kisasi, kaunti ya Kitui .

Kwa mjibu wa naibu chiifu wa Masimbini Mulu Kalu , aliyejeruhiwa ni dadake marehemu  na alipelekwa katika hospitali ya Kitui Level 4 kwa matibabu.Ajali hiyo ilitokea kwenye Barabara ya Kibwezi kuelekea -Kitui  wakati gari husika lilikuwa likitoka  Mutomo kuelekea  Kitui.

Wakati huo huo Mwanamume mwenye umri wa miaka arobaini ameuawa hivi leo, katika ajali ya kugonga na kukimbia alipokuwa akijaribu kuvuka barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Cheptiret kaunti ya Uasin Gishu.

Walioshuhudia wanasema marehemu alionekana mlevi kabla ya kujaribu kuvuka barabara karibu na daraja la Cheptiret alipogongwa na gari lililokuwa likienda kasi.

Walioshuhudia wanasema mtu huyo alifariki dunia papo hapo na kwamba gari lililomgomga halikusimama Baada ya tukio hilo.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Ainabkoi Stephen Kimunya amedhibitisha  kisa hicho cha  leo asubuhi , akisema polisi wanachunguza kisa hicho ili kumpata dereva ambaye bado hajakamatwa.Wakati huo huo, mwili wa marehemu umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Moi.

 

 

 

December 26, 2023