watoto

Maafisa wa polisi katika eneo la Kilifi wamewatia nguvuni mwanaume na mke wake, wanaodaiwa kuhusika na vifo vya watoto wao wawili kwa kukataa kuwapeleka hospitalini ili kupokea huduma za matibabu. Tukio hili la kusikitisha limejitokeza baada ya wazazi hao kukataa kuwapeleka hospitalini watoto wao waliokuwa na umri wa miaka 13 na 11, licha ya kuwa walikuwa wanaugua. Wazazi hao walidai kuwa dini yao inawazuia kuenda hospitalini.

Maafisa wa polisi walifanya operesheni na kuwakamata wazazi hao hii leo. Kwa mujibu wa taarifa, mmoja wa watoto hao alifariki dunia siku ya Jumamosi, na mwenzake alifariki siku ya Jumapili, akiwa mikononi mwa mhubiri mmoja ambaye naye pia amekamatwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.

Mkuu wa Polisi wa Kilifi Kaskazini, Kenneth Maina, amethibitisha tukio hili na kusema kuwa watoto hao walikuwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Kilimo katika eneo hilo. Uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa ili kubaini hasa killichosababisha vifo vya watoto hao.

 

September 20, 2023