Mitihani

Serikali ya Kenya imechukua hatua za dharura kwa kushirikiana na idara mbalimbali na serikali za kaunti, ili kuhakikisha kuwa maandalizi ya mitihani ya kitaifa yanafanyika kwa ufanisi mwishoni mwa muhula huu. Hatua hii inakuja wakati ambapo maeneo mengi ya taifa yanatarajiwa kukumbwa na mvua kubwa baada ya kuanza kwa mvua za El Nino mwezi ujao.

Katibu wa Elimu ya Msingi nchini, Belio Kipsang, ameeleza kuwa serikali inaendelea na juhudi za kubaini maeneo ambayo yanaweza kukabiliwa na hatari ya mafuriko kutokana na mvua hizo. Kipsang amethibitisha kuwa serikali itashirikiana kikamilifu na idara za usalama kama vile idara ya polisi na Jeshi ili kuhakikisha kuwa mitihani inasambazwa kwa usalama katika maeneo yote.

Akizungumza katika shule ya upili ya Shimo la Tewa katika kaunti ya Mombasa baada ya kutoa maelekezo kwa washikadau wa elimu, Katibu huyo amesema kuwa wanafunzi wote, hususan wale wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za usalama, watahakikishiwa usalama wao kabla, wakati, na baada ya kipindi cha mitihani hiyo.

Mwaka huu, takriban wanafunzi milioni 1.4 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KCPE, wakati wanafunzi milioni 1.2 watatahiniwa katika mtihani wa KPSEA. Aidha, idadi ya watakaotahiniwa kwenye mtihani wa KCSE itakuwa karibu laki tisa.

 

Share the love
September 20, 2023